Katika mchango wake, Mhe. Kessy aliongea kwa uchungu na hisia kali akilalamikia jinsi mafisadi wanavyodidimiza uchumi wa nchi na alilieleza Bunge kuwa anatamani makaburi ya mafisadi yafukuliwe na wafungwe minyororo ili iwe fundisho kwa wengine. Mhe. Kessy aliliambaia bunge kuwa “Mimi nilikuwa Bunge la nne hapa ndugu zangu, nilikuwa msumari nazungumza ukweli kuhusu mafisadi, wezi wa mali ya umma, nilizungumza mpaka makaburi yao yafukuliwe wafungwe minyororo kwenye makaburi”.

Mhe. Kessy alienda mbali zaidi kwa kuzungumzia safari za Wabunge kwenda nchi za nje huku wengine wakirudia uwanja wa ndege kitendo alichokiita ubadhirifu wa mali ya umma kwa vile hazikuwa na tija kwa Bunge. Mhe. Kessy aliliambaia Bunge “Nilizungumza vilevile safari za Wabunge kwenda nje, hazina manufaa, tunapishana airport kama wakimbizi…hizi safari hazifai…wengine walikuwa wanarudia airport”.

Mhe. Kessy aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa vile ameidhibiti na kuinyoosha nchi na alitaka aongeze kasi zaidi kupambana na mafisadi na wala rushwa nchini. Aliliambia Bunge kwamba alimwambia Rais spidi yake bado hajaiona na kwamba nchi hii bado ina mafisadi wengi wanaotuibia.

Mhe. Kessy, kama kawaida yake anapochangia hoja Bungeni, haachi vichekesho kwa Wabunge wenzake, safari hii, alipokuwa analaani kitendo cha baadhi ya Wasanii kutunga nyimbo za matusi kumtukana Rais, alisema ” Wangeniachia mimi dakika mbili niwanyooshe hawa”, kitendo kilichofanya Wabunge wampigie makofi kumshangilia.

Kwa siku kadhaa, mjadala wa Wasanii kuimba nyimbo zenye maudhui ya kumtukana Rais na mmoja wao Nay wa Mitego kukamatwa na kushikiliwa na polisi ulitawala Bungeni na kwenye mitandao ya kijamii lakini Rais Mhe. Dkt.Magufuli alitoa agizo Msanii Nay wa Mitego aachiwe huru na Polisi kwa kitendo cha wimbo wake unaojulikana kwa jina la WAPO wenye mashairi ya kumtukana Mhe. Rais. Mhe. Rais Dkt. Magufuli aliagiza kuwa wimbo huo wa WAPO upigwe kwenye vituo vyote vya redio na televisheni pamoja na kumbi za starehe ila auboreshe ikiwezekana uwekwe vionjo vingine kama vile mapambano dhidi ya rushwa.

Hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliwasilishwa Bungeni Aprili 9, 2017ambapo Waziri Mkuu alilieleza Bunge mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya rushwa kiasi cha kutambulika na mashirika ya Kimataifa yanayojishughulisha na tafiti kuhusu masuala ya rushwa Duniani. Shirika la Transparency International (TI) katika utafiti wake wa mwaka 2016 limesema kuwa viwango vya rushwa vinapungua nchini Tanzania.

Aidha, Mhe. Waziri Mkuu, alilieleza Bunge kuwa, katika kipindi cha 2016/2017, TAKUKURU katika operation zake iliokoa kiasi cha shilingi bilioni 9.75 hadi kufikia mwezi Februari 2017 na kufikia mwezi Machi 2017, fedha iliyookolewa na TAKUKURU na kurejeshwa serikalini ni shilingi Bilioni 12.316.

Akihitimisha hotuba yake Aprili 11, 2017, Waziri Mkuu aliliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi 171,664,055,000 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake pamoja na jumla ya shilingi 121,652,262,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018. Fedha hizo ziliidhinishwa na Bunge.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuhitimisha hoja ya Ofisi yake kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2017/2018 na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2016/2017