Idara ya Utafiti na Udhibiti ni moja ya idara tano zinazounda TAKUKURU. Jukukmu lake la msingi /dhima yake ni “KUZUIA RUSHWA KWA KUIMARISHA MIFUMO”. Idara hii inaoongozwa na falsafa ya “Kuzuia ni Bora na nafuu kuliko Kutibu’. Idara inaamini kuwa kutibu matokeo ya rushwa ni gharama zaidi lakini pia ni vigumu kuliko kuzuia. Uzuiaji huu hufanyika kwa kuimarisha Mifumo, Sera na Taratibu za utendaji kazi katika sekta za umma na zile za binafsi. Kuzuia badala ya kutibu kuna faida kubwa tatu. Kwanza, Serikali itaokoa raslimali fedha na muda ambao ungetumika katika kukabiliana na matokeo ya rushwa baada ya kuwa imetendeka. Pili, mifumo/taratibu za utoaji huduma muhimu za kijamii ikiimarishwa kwa kuziba mianya yote, vita dhidi ya rushwa itapata ufanisi mkubwa na hivyo kupunguza au kulimaliza kabisa tatizo la rushwa nchini. Tatu, mapambano dhidi rushwa yasipolenga katika kutokomeza na kuharibu vyanzo vyake vya asili vilivyomo kwenye mifumo mbalimbali ya utoaji huduma (root causes), Serikali inaweza kutumia nguvu kubwa lakini matokeo yake yanaweza yasiwe ya kuridhisha kwa sababu ya kutoziba mianya. Aidha, kuzuia na kuidhibiti rushwa kabla haijatendeka, kutasaidia kuongeza kasi ya Serkali katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuondoa umaskini; na hivyo kusaidia kufikiwa kwa lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati (middle income economy) ifikapo mwaka 2025.

JUKUMU LA IDARA KISHERIA

Kwa mujibu wa kifungu cha 7 (a) na (c) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007, idara inalo jukumu na kufanya tafiti na dhibiti kwa kupitia mifumo na taratibu mbalimbali zinazoongoza utendaji wa Taasisi na mashirika ya Umma na Taasisi zisizo za Serikali ili kupima uzingatiaji na utekelezaji wa Sheria, Taratibu na Miongozo mbalimbali kwa lengo la kubaini mianya au vitendo vya rushwa; kuzishauri Taasisi za Serikali na binafsi juu ya namna bora ya kuzuia rushwa na kusimamia utekelezaji wa mifumo na taratibu zilizorekebishwa baada ya kubainika kwa mianya ya rushwa.

Kimuundo, Kurugenzi inaongozwa na Mkurugenzi akisaidiwa na Wakuu wa Sehemu wawili; Mkuu wa sehemu ya Utafiti na Mkuu wa sehemu ya Udhibiti. Ili kuleta utendaji makini na wenye tija sehemu hizo zimegawanyika katika timu, ambazo hutenda kazi chini ya Wakuu wa Timu. Aidha, kupitia Wakuu wa Madawati waliopo katika ofisi zetu za Mikoa na Wilaya zote za Tanzania Bara, Kurugenzi ya Utafiti na Udhibiti imekuwa ikiratibu kazi za kuzuia na kudhibiti rushwa katika mifumo mbalimbali hadi kufikia kwenye ngazi za chini za utawala na utendaji (Vijiji/Mitaa/Vitongoji).

Jukumu kubwa la Sehemu ya Utafiti ni kubuni na kuandaa mapendekezo ya kufanya tafiti mbalimbali zenye lengo la kubaini vitendo vya rushwa katika sekta za umma na binafsi ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umma. Matokeo ya tafiti hizo hujadiliwa na wadau mbalimbali na hatimaye kuwekewa mikakati ya pamoja na wadau kama njia shirikishi ya kuleta mabadiliko chanya katika maeneo husika.

Aidha, Sehemu ya Udhibiti inahusika na uchambuzi wa Mifumo ya utoaji huduma katika Taasisisi na Idara mbalimbali za umma na zile za binafsi. Baada ya uchambuzi kukamilika, idara inalo jukumu la kuandaa Warsha kwa lengo la kuwakutanisha wadau ili kujadili kwa pamoja matokeo na kasha kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kuitekeleza. Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa kupitia Kurugenzi yake ya Utafiti na Udhibiti imefanya kazi nyingi ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika Taasisi, Idara na Sekta za umma na binafsi nchini. Baadhi ya kazi nyingi na nzuri zilizofanywa na Kurugenzi hii ni: (open the folder attached: TAARIFA ZA TAFITI”)