Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007 inaipa TAKUKURU mamlaka ya kuwa chombo huru cha kuongoza mapambano dhidi ya rushwa Tanzania Bara kwa kutoa elimu kwa umma, kuzuia, kuchunguza rushwa, na kufungua mashtaka.

Majukumu ya Jumla ya TAKUKURU ni kuchukua hatua zinazofaa kwa lengo la kuzuia na kupambana na rushwa katika idara za serikali, mashirika ya umma na taasisi binafsi nchini. Ili kutekeleza majukumu haya, kazi za TAKUKURU, kama zilivyoorodheshwa katika kifungu cha 7 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007, itakuwa ni pamoja na :

Kufanya uchambuzi na kutoa ushauri wa kitalaam juu ya mienendo na taratibu mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli za umma, mashirika ya umma, na taasisi binafsi nchini kwa lengo la kuifanya kazi ya kung’amua au kuzuia rushwa kuwa ya ufanisi pamoja na kurahisisha kazi ya upitiaji wa kanuni au taratibu za kufanya kazi ambazo zinaboresha ufanisi na uwazi  wa taasisi husika.

Kuanzisha na kustawisha ushirikiano na ushiriki wa umma katika mapambano dhidi ya rushwa.

Kutoa ushauri kwa jamii, idara za serikali, mashirika ya umma, na taasisi binafsi kuhusu njia na mbinu muafaka za kuzuia vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuboresha mikakati na taratibu za kazi katika idara za serikali, mashirika ya umma na taasisi binafsi ili kuwezesha kupambana na vitendo vya rushwa katika idara na taasisi huska.

Kushirikiana na taasisi za ndani na nje ya nchi zinnazojihusisha na mapambano ya rushwa.

Kuchunguza/kupeleleza na kuendesha mashtaka dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa. Hata hivyo, uendeshaji wa mashtaka ya rushwa utafanyika kwa mujibu wa maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini.

Kuchunguza/kupeleleza malalamiko yoyote yanayohusiana na kufanyika au njama za kufanyika kwa makosa yaliyoorodheshwa katika sheria hii na hata mwenendo wa kiongozi wa umma wenye dalili za rushwa.

Idara za TAKUKURU

Ili kutekeleza mamlaka na majukumu yake, TAKUKURU ina idara tano ambazo zinaongozwa na Wakurugenzi. Idara hizi ni :

Idara ya Uchunguzi ambayo inashughulikia kubaini vitendo vya rushwa, kuuchunguza na kuendesha mashtaka dhidi ya watuhumiwa wa vitendo vya rushwa

Idara ya Elimu kwa Umma ambayo ina jukumu la kuishirikisha jamii katika mapambano dhidi ya rushwa

Idara ya Utafiti na Udhibiti ambayo ina jukumu la kuzuia vitendo vya rushwa kwenye sekita za umma na binafsi kupitia uimarishaji wa mifumo

Idara ya Mipango, Ufuatiliaji na Tathimini ambayo inajukumu la kuiwezesha taasisi kuwa na mifumo madhubuti na endelevu ya mipango,bajeti,takwimu,ufuatiliaji na tathimini

Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu ambayo ina jukumu la kuziwezesha idara nyingine zote nne kwa kuzipatia wafanyakazi wenye sifa, vifaa na vitu vingine.

.